Ticker

6/recent/ticker-posts

BoT YANG'ARA SABASABA, YATWAA TUZO YA BANDA BORA

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeibuka mshindi wa kwanza wa banda bora katika kundi la Taasisi za Usimamizi kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (Saba Saba), yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2026.

Tuzo hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, katika hafla ya kufunga maonesho hayo iliyofanyika leo, tarehe 13 Julai 2026. Kwa niaba ya Benki Kuu ya Tanzania, tuzo hiyo ilipokelewa na Meneja Msaidizi, Idara ya Mawasiliano BoT, Bi. Noves Moses.

Ushindi huo unatokana na ubora wa maandalizi ya banda la Benki Kuu pamoja na huduma za elimu kwa umma zilizotolewa kwa wageni waliotembelea banda hilo katika kipindi chote cha maonesho.

Kupitia banda lake, Benki Kuu ilitoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake ya msingi katika kusimamia ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa, ikiwemo utekelezaji wa sera ya fedha, kudumisha uthabiti wa bei, kusimamia sekta ya fedha na mifumo ya malipo, pamoja na kuhamasisha ujumuishi wa kifedha kwa maendeleo ya wananchi na uchumi kwa ujumla.

Katika kipindi chote cha maonesho, banda la Benki Kuu ya Tanzania lilitembelewa na zaidi ya wananchi 15,000, wakiwemo viongozi mbalimbali wa Serikali, wawakilishi wa taasisi za umma na binafsi, mabalozi, wanafunzi na wadau wengine. Wageni hao waliopata fursa ya kupata elimu, kuuliza maswali na kupatiwa ufafanuzi kuhusu shughuli na huduma zinazotolewa na BoT.

Tuzo hiyo ni uthibitisho wa ubunifu, weledi na kujituma kwa watumishi wa BoT walioshiriki katika maandalizi na uendeshaji wa banda hilo. Aidha, inaakisi dhamira ya Benki Kuu ya kuendelea kutoa huduma bora kwa umma, kuimarisha mawasiliano na wadau wake, na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, kwa wakati na kwa uwazi kuhusu sera, majukumu na huduma mbalimbali zinazotolewa na BoT.

Post a Comment

0 Comments