Ticker

6/recent/ticker-posts

KATAMBI AWAHIMIZA WAWEZESHAJI STADI ZA MAISHA KUTOA ELIMU KWA VIJANA


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akizungumza wakati hafla ya kufunga mafunzo ya stadi za maisha (Life Skills) kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu katika ukumbi wa Midland hoteli, mkoani Mwanza, Disemba 17, 2022.


Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya stadi za maisha (Life Skills) wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akikabidhi cheti kwa Mkufunzi wa Chuo cha VETA – Mwanza, Bw. Bakari Mahundu (kulia) wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo.


Afisa Maendeleo ya Vijana Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Godfrey Massawe akieleza jambo wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya stadi za maisha (Life Skills) kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu yaliyofanyika katika ukumbi wa Midland hoteli, mkoani Mwanza, Disemba 17, 2022.

********************

Na: Mwandishi Wetu – MWANZA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amewataka wawezeshaji stadi za maisha kuhakikisha elimu hiyo inawafikia vijana wasio na Ulemavu na wenye Ulemavu ili waweze kutambua uwezo wao wa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za ujenzi wa Taifa.

Naibu Waziri Katambi ametoa agizo hilo leo Disemba 17, 2022 wakati akifunga mafunzo ya stadi za maisha (Life Skills) kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu katika ukumbi wa Midland hoteli, mkoani Mwanza huku akieleza lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa elimu ya stadi za maisha inajumuishwa kwenye afua na programu za kushughulikia changamoto za vijana ikiwemo vijana wenye Ulemavu.

Amesema kuwa, elimu ya stadi za maisha ni muhimu kwa kuwa inawajenga vijana na kuwapatia mbinu na maarifa ambayo yatawasaidia kutambua fursa zilizopo, namna ya kuweza kuzifikia na kujikwamua kiuchumi.

“Vijana wakipatiwa elimu ya stadi za maisha watahamasika kuwa na mabadiliko chanya ya tabia, mienendo na mitazamo. Natumaini mtatumia elimu hii kuhakikisha kwamba kunakuwa na mafunzo ambayo yatawasaidia vijana kuwa na mbinu na maarifa mbalimbali zitakazo wawezesha kujitambua, kuwa na uthubutu na kufanya maamuzi sahihi,”

Ameongeza kuwa, ifikapo mwaka 2023 idadi ya waelimishaji wa stadi za maisha kitaifa inatarajiwa kufika 352 kutoka idadi ya wawezeshaji 142 waliopo kwa takwimu za mwaka 2022, ongezeko hilo itakuwa sawa na 60.2% ya lengo lililokusudiwa, hivyo kutakuwa na ongezeko kubwa la idadi ya waelimishaji rika wanaotarajiwa kutoa elimu ya stadi za Maisha kwa vijana wengi zaidi.

Aidha, Naibu Waziri katambi amesema kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kushughulikia masuala mbalimbali ya Watu wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeendelea kusimamia na kutekeleza maagizo yanayotolewa na viongozi mbalimbali ikiwemo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika kuimarisha ustawi wa Watu wenye Ulemavu nchini, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya stadi za maisha kwa vijana wenye Ulemavu ili waweze kujitambua, kuwa na uthubutu, kufanya maamuzi sahihi na kuepuka vishawishi pamoja na mazingira hatarishi.

Sambamba na hayo ameeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha Vyuo vya Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu sita ikiwemo Yombo – Dar es Salaam, Luanzari - Tabora, Mtapika - Mtwara, Sabasaba - Singida, Mirongo – Mwanza na Masiwani – Tanga. Sambamba na ujenzi wa vyuo vipya 3 katika mkoa wa Songwe, Ruvuma na Kigoma.

“Ni wajibu wetu kuwatambua Watu wenye Ulemavu, kuwasikiliza na kuwahudumia,” amesema

Pia, ameshukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuwezesha kutoa mafunzo hayo ya stadi za maisha (Life Skills) kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu.

Naye, Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mwanza, Bw. Daniel Machunda ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana kwa kutoa mafunzo hayo katika mkoa huo ikiwa ni pamoja na zoezi la majaribio ya Mwongozo wa Stadi za Maisha kwa vijana wa halmashauri ya Nyamagana na Ilemela ambapo mafunzo hayo yalifanyika disemba 5 hadi 9, 2022.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho Sabasaba, mkoani Singida, Bi. Fatuma Malenga amesema kuwa elimu ya stadi za maisha waliyopata wataitumia vyema kwa kuwajengea vijana uwezo ili waweze kujitambua, kuwa na uthubutu na kufanya maamuzi sahihi.

Post a Comment

0 Comments