Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA MATAPELI WANAOSAMBAZA TAARIFA ZA UONGO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumzia uamuzi wa Serikali wa kuwachukulia hatua matapeli wanaosambaza taarifa za uongo kuhusu kuwarejesha katika Utumishi wa Umma watumishi waliobainika kughushi vyeti na kuondolewa katika Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara.

*****************************

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 27 Januari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali inawafuatilia ili kuwachukulia hatua matapeli wanaosambaza taarifa za uongo kuhusu kuwarejesha katika Utumishi wa Umma watumishi waliobainika kughushi vyeti na kuondolewa katika Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara.

Mhe. Jenista ameeleza uamuzi huo wa Serikali kufuatia matapeli wanaoendelea kusambaza taarifa za uongo zikiainisha kuwa Serikali imefanya uamuzi wa kuwarejesha watumishi walioondolewa kazini kwa kosa la kughushi vyeti.



Mhe. Jenista amefafanua kuwa, mara kadhaa ofisi yake imekuwa ikikanusha taarifa ya uongo inayotolewa na matapeli kwa masilahi yao binafsi, taarifa ambayo imekuwa ikibadilishwa tarehe mara kwa mara lakini maudhui ni yale yale.



Ameongeza kuwa, taarifa hiyo ya uongo ambayo imekuwa ikisambazwa kupitia mitandao ya kijamii, imezua taharuki miongoni mwa jamii, imetengeneza mianya ya rushwa kwa wahusika, imesababisha wahusika kutapeliwa kwa madai ya kusaidiwa kurejeshwa katika utumishi wa umma, imewaletea usumbufu wahusika na kuwagharimu kusafiri kwa lengo la kukamilisha mchakato wa kurejeshwa katika Utumishi wa Umma.



Kufuatia usumbufu huo unaotokana na usambazaji wa taarifa za uongo, Mhe. Jenista ametoa onyo kwa matapeli wanaoendelea kuupotosha umma kuacha mara moja kitendo hicho na kuongeza kuwa watakaoendelea kukiuka, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.



Aidha, Mhe. Jenista ametoa pole kwa wote waliopata usumbufu kutokana taarifa hiyo ya uongo na kuwataka kuwa makini dhidi ya matapeli hao.



Mhe. Jenista amewataka watumishi wa umma na wadau wa utumishi wa umma kuzingatia njia sahihi za kupata taarifa za kiutumishi ambazo zimekuwa zikitumiwa na waajiri kuwafikishia taarifa.

Post a Comment

0 Comments