Ticker

6/recent/ticker-posts

BENKI YA DUNIA YAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA TANZANIA


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa kikao na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, Makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Washington D.C, Marekani, ambapo Benki hiyo imeahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika kufanikisha ajenda yake ya kukuza uchumi na maendeleo.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, akizungumza wakati wa mkutano na Ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (hayupo pichani), ambapo aliahidi kuwa Benki yake itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika kufanikisha malengo yake ya kukuza uchumi na kuwahudumia wananchi wake huku akipongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kusimamia uchumi. Kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bw. Nathan Belete.
Waziri wa Fedha na Mipango na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa pili kushoto) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum (kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia-Tanzania, Bw. Nathan Belete, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo Jijini Washington D.C, Marekani, wakati wa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)


Waziri wa Fedha na Mipango na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango=Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum (wa pili kulia), na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, wakiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia-Tanzania, Bw. Nathan Belete, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo wakati wa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Jijini Washington D.C, Marekani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum (kushoto) akisalimiana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, wakati wa mikutano ya kipupwe iliyoandaliwa na Benki ya Dunia na Shrika la Fedha la Kimataifa (IMF), jijini Washington D.C, Marekani. Katikati ni Kiongozi wa Ujumbe huo wa Tanzania, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, akiwa katika picha na Meneja Uendeshaji wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bi. Preeti Arora, baada ya kufanyika mazungumzo kati ya Benki ya Dunia na ujumbe wa Tanzania, wakati wa mikutano ya kipupwe iliyoandaliwa na Benki hiyo na Shrika la Fedha la Kimataifa (IMF), jijini Washington D.C, Marekani. Nyuma ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto), akiteta jambo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Washington DC, Marekani)


*********************


Na Benny Mwaipaja, Washington, DC


MAKAMU Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, ameahidi kuwa Benki yake itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika kufanikisha malengo yake ya kukuza uchumi na kuwahudumia wananchi wake huku akipongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kusimamia uchumi wake.


Bi. Kwakwa ametoa pongezi hizo Jijini Washington D.C nchini Marekani, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, kwenye mikutano ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.


Alisema kuwa uchumi wa Tanzania umekuwa tulivu na umekua kwa kasi ikilinganishwa na nchi nyingine anazozisimamia zilizoko Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, ambazo zinahaha kujikwamua kiuchumi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo msukosuko wa uchumi unaotokana na vita baina ya Urusi na Ukraine, pamoja na madhara ya UVIKO-19


Aliishauri Serikali kuendelea kusimamia kikamilifu sera nzuri za fedha na uchumi zinazoleta utulivu kwenye uchumi na kuhakikisha inaendelea kudhibii mfumuko wa bei pamoja na kuweka mipango endelevu ya kuishirikisha zaidi sekta binafsi katika shughuli za kiuchumi.


Bi. Kwakwa aliahidi kuwa Benki yake itaendelea kuipatia fedha Tanzania kupitia madirisha mbalimbali ili iweze kutekeleza miradi mbalimbali inayoweza kuchochea ukuaji wa uchumi kwa haraka, ikiwemo sekta za nishati, kilimo, maji na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya kukuza uchumi wa tai ana wananchi kwa ujumla.


sema kuwa Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia alisema kuwa mfumuko wa bei ni kama kodi mbaya inayowaumiza zaidi wananchi masikini na kwamba Benki yake itaitua Tanzania kama kielelezo na mfano wa kuigwa nan chi nyingine duniani.


Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Benki ya Dunia kwa pongezi hizo kwa usimamizi mzuri wa sera za uchumi na fedha na kuahidi kumfikishia pongezi hizo Mheshimiwa samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Aidha, Dkt. Nchemba alirejea kutoa shukrani zake kwa Benki hiyo kwa msaada mkubwa wa ushauri wa kitaalam na rasilimali fedha, unaotolewa na Benki hiyo kwa Tanzania na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi na hivyo kupunguza umasikini wa watu wake.


Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salum Mkuya, alisema kuwa Benki ya Dunia ni mdau mkubwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kusaidia fedha na misaada inayotumika kuboresha sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.


Alisema kuwa hivi sasa, Zanzibar, inafanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia sera ya uchumi wa buluu ikiwemo matumizi ya bahari na sekta ya utalii na kwamba Benki ya Dunia ni mdau mkubwa wa kufanikisha sera hiyo ambayo imelenga kuikwamua jamii ili iondokane na umasikini.






Post a Comment

0 Comments