Ticker

6/recent/ticker-posts

MJUMBE WA KAMATI KUU CCM TAIFA, MHE.HEMED SULEIMAN AWATAKA VIONGOZI WA CCM KUSINI PEMBA KUDUMISHA UPENDO BAINA YAO


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe . Hemed Suleiman Abdulla amewataka Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba kushirikiana Pamoja na kudumisha upendo baina yao ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mhe. Hemed ametoa wito huo wakati akiwasalimia wanachama wa CCM pamoja na kutoa Iftar kwa watendaji wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba katika Ofisi za CCM Mkoa wa Kusini Pemba zilizopo CHACHANI Chake chake Pemba.

Mhe. Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ni wajibu wa kila kiongozi kuwasaidia watendaji ili kuleta ufanisi mzuri wa kazi katika kukijenga Chama hicho.

Amesema ameamua kutoa mchele kilo ishirini na tano (25) kwa kila mtendaji wa Chama na Jumuiya zake Katika mkoa huo kwa lengo la kuwasaidia watendaji wa Chama cha Mapinduzi waweze kufanya kazi kwa ufanisi mzuri na kutimiza malengo waliojiwekea.

Aidha Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuacha majungu, fitna na makundi yasiokuwa na tija kwa mustakabali wa Chama na Taifa kwa ujumla.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewapongeza Viongozi waliochaguliwa katika chaguzi zilizofanyika katika ngazi ya shina hadi Taifa na kuwataka kuwa na mashirikiano na wanaowaongoza ili kuweza kufikia shabaha ya Chama Cha Mapinduzi na kusema kuwa safu imetia kazi iendelee.

Akitoa shukrani Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba Ndg YUSSUF ALI JUMA amemshukuru Mhe. Hemed kwa uamuzi wake wa kuwasaidia watendaji wa CCM katika mkoa huo na kueleza kuwa kufanya hivyo kutaleta ufanisi mzuri wa kazi kwa watendaji na kusisitiza kuwa kitendo hicho kina thibitisha uwezo wake wa kuongoza kwa vitendo.

Aidha ameahidi kuwa watasimamia miongozo yote yanayotolewa na viongozi wakuu kwa lengo la kukisaidia Chama Cha Mapinduzi kiweza kuendelea kushika hatamu siku hadi siku.

Post a Comment

0 Comments