Ticker

6/recent/ticker-posts

TUME HAKI JINAI YAKUTANA NA MABALOZI JIJINI DAR ES SALAAM

Tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini imekutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na kuwapa taarifa ya hatua iliyofikiwa na tume hiyo.

Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohammed Othman Chande, amesema tume imekutana na mabalozi hao kwa lengo la kuwapa taarifa ya hatua iliyofikiwa na tume hiyo wakiwa ni sehemu ya wadau.

"Taasisi za Kimataifa wakati mwingine zinafanya kazi na taasisi za haki jinai, tumeona tuwafahamishe kwa kuwa nao ni wadau. Pia tunawakaribisha watoe mapendekezo yao kwa sababu huu sio mwisho wa kupokea maoni," alisema Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Chande.

“Kwa sasa tunamalizia uchambuzi wa maoni yaliyokusanywa, kazi ambayo inatarajiwa kufanyika kwa mwezi mmoja na baadaye itatolewa rasimu ya mapendekezo,” alisema Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Chande na kuongeza kuwa rasimu ya mapendekezo itahusisha yanayopaswa kutekelezwa haraka, kwa muda wa kati na kwa muda mrefu.

Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Chande, alisema kuwa shauku ya wananchi ni kuwa na imani na taasisi za haki jinai nchini na kinachofanywa na tume hiyo kinalenga kufanikisha hilo.

"Shauku kubwa ya wananchi ni kuona mageuzi katika taasisi za haki jinai na tunatarajia mapendekezo yetu yafanikishe hilo," alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Chande.

Kwa kipindi cha miezi mitatu takriban wananchi 10,000 wamesikilizwa, mikutano 25 ya hadhara, imefanyika katika Wilaya 53 na Mikoa 25 na tume imefanikiwa kuwasikiliza wadau mbalimbali.

Akifungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab alisema tume hiyo iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuangalia njia bora ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini.

Alisema tume hiyo ina jukumu la kuangalia changamoto zinazokabili taasisi za haki jinai na kupendekeza uboreshaji wa mfumo wa haki jinai nchini.

Balozi Fatma Rajab alifafanua kuwa tume kama hiyo zimekuwa zikiundwa tangu uhuru wa Tanganyika na maboresho mbalimbali yamefanyika nchini ikiwa ni matokeo ya tume hizo.

"Tume hii tunatarajia ije na mapendekezo yatakayoboresha mfumo wa haki jinai kulingana na mahitaji ya sasa," alisema Balozi Fatma.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Fatma ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mfumo wa haki jinai nchini unaboreshwa na kuwa imara zaidi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akiwasilisha hotuba yake wakati wa mkutano baina ya Tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akiwasilisha hotuba yake wakati wa mkutano baina ya Tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohammed Othman Chande akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akiongoza mkutano wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Mhe. Manfredo Fanti akichangia jambio wakati wa mkutano wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Norway Nchini Mhe. Elisabeth Jacobsen akichangia jambio wakati wa mkutano wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam
Baadhi ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wakifuatilia mkutano baina yao na tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini Jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohammed Othman Chande (kulia) pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (kushoto) wakifuatilia mkutano

Mwenyekiti wa tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohammed Othman Chande pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab pamoja na wajumbe wa tume hiyo katika picha ya pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa

Post a Comment

0 Comments