MIXX BY YAS, COPRA NA YAS WAUNGANA KUFANYA SEKTA YA KILIMO KIDIJITALI

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam, 09 Julai 2025 — Katika hatua ya kihistoria ya kuwawezesha wakulima wa Tanzania na kuboresha sekta ya kilimo, Mixx by YAS, Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mengine (COPRA), na Yas wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati yenye lengo la kubadilisha jinsi wakulima watakavyopata taarifa za masoko, bei ya mazao, na malipo kupitia majukwaa ya kidijitali.
Hafla ya utiaji saini, iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo, ni mfano mzuri ambapo sekta binafsi na umma zinaweza kuungana kwa dhamira ya pamoja ya kutumia ubunifu na teknolojia kama kichocheo cha maendeleo jumuishi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Angelica Pesha, Mkurugenzi Mtendaji wa Mixx by Yas, alisema kuwa ushirikiano huo unaashiria mwanzo wa sura mpya kwa wakulima wa Tanzania.
“Leo hatusaini tu mkataba - tunaandika historia mpya ya kilimo cha Tanzania. Kupitia Mixx by Yas, wakulima sasa wataweza kupata taarifa za bei sokoni kwa wakati halisi, kuuza na kununua mazao kidijitali, na kupokea malipo ya papo hapo moja kwa moja kwenye simu zao za mkononi kwa njia ambayo ni rahisi na salama. Hii ndiyo maana halisi ya uwezeshaji wa kidijitali,” alisema Pesha.

“Lengo letu ni kuhakikisha kila mkulimabila kujali alipoanapata nyenzo na taarifa zinazohitajika ili kufanikiwa katika soko la ushindani. Tunaanza na maeneo 10 muhimu ya kilimo, ambapo tayari tumeshafunga skrini/TV kuonyesha taarifa za bei moja kwa moja na vipindi vya elimu. Lakini hatuishii hapo: Tutaongeza huduma za intaneti hadi katika maeneo ya vijijini yasiyo na huduma zetu, tutafunga minara ya mawasiliano na kushirikiana na Serikali za mitaa kutoa mafunzo ya uelewa TEHAMA kwa wakulima.

Kwa muda mrefu, wakulima wetu wameachwa nyuma katika uchumi wa kidijitali kutokana na ukosefu wa miundombinu na taarifa kwa wakati. Ushirikiano huu unabadilisha hali hiyo. Hatujengi tu jukwaa la kidijitali; tunajenga mfumo shirikishi, unaounganishwa na unaoongozwa na data unaowaunga mkono wakulima, kuimarisha ushirika na kuwezesha maamuzi ya kisera yenye maarifa kwa watunga sera na wawekezaji. Huu ni mwanzo wa safari ya mabadiliko na tunaisafiri pamoja.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Bi. Irene M. Mlola, aliusifu mpango huo, akiuelezea kama hatua ya mageuzi katika kuziba pengo la taarifa na upatikanaji ambalo limekuwa changamoto kwa wakulima wa vijijini kwa muda mrefu.

“Kwetu sisi COPRA, ushirikiano huu ni kichocheo muhimu cha kuleta imani, uwazi na ujumuishaji katika minyororo ya thamani ya mazao ya Tanzania,” alisema Bi. Mlola.

“Ushirikiano wetu unahakikisha kuwa wakulima wadogo hawataachwa nyuma tena. Kupitia upatikanaji wa bei kwa wakati halisi, malipo salama, na mifumo iliyopangwa ya kidijitali, tunajenga soko ambapo wakulima wadogo wanapata fursa sawa na ya haki. Hiki ndicho kilimo cha kisasa tunacholenga na tunakifanya kwa pamoja.”

Aliongeza kuwa ushirikiano huu unaendana na maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuiweka Tanzania kama ghala la chakula la kanda kwa kutumia ubunifu katika kurasimisha masoko na kuongeza ushindani.

Post a Comment

0 Comments