Katika jitihada za kuboresha sekta ya elimu nchini Tanzania, ADEM na Taasisi ya Project Zawadi wameingia makubaliano ya ushirikiano utakaowezesha kuendesha mafunzo ya muda mfupi kuhusu uongozi, usimamizi na uendeshaji wa elimu kwa viongozi wa Mkoani Mara.
Ushirikiano huu unalenga kuwajengea uwezo viongozi wanaosimamia sekta ya elimu kuanzia ngazi ya shule hadi Mkoa
Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya ADEM na Project Zawadi, Mtendaji Mkuu Dkt. Maulid J. Maulid amesema lengo la Makubaliano hayo ni kuweka msingi wa ushirikiano baina ya Taasisi hizo mbili kwa ajili ya kuandaa na kutekeleza programu za mafunzo ya muda muda mfupi kuhusu uongozi na usimamizi wa elimu nchini.
“Ili taasisi zenye majukumu yanayofanana ziweze kuboresha utendaji wake ni muhimu kuepuka kufanya kazi kwa kujitenga, zinahitaji kujenga ushirikiano na uhusiano katika kuimarisha utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi na kuleta tija na manufaa kwa taasisi husika na Serikali kwa ujumla. Kwa kuwa rasilimali za Serikali katika eneo la utoaji wa mafunzo kwa viongozi wa elimu bado hazitoshelezi hivyo ni vyema taasisi zisizo za Serikali kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuhakikisha zinasaidia kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu kwa kuwezesha mafunzo hayo kama walivyofanya taasisi ya Project Zawadi katika mkoa wa Mara ambapo katika kutekeleza hilo wameamua kushirikiana na ADEM”.
Nae Mkurugenzi Mkaazi Project Zawadi nchini Bw. Raymond Gilbert akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa Taasisi yake inaamini katika ujuzi, utaalamu na uwezo wa ADEM katika kuleta mabadiliko chanya kwenye eneo la uongozi na usimamizi wa elimu kwa kuwajengea uwezo viongozi mbalimbali wa elimu nchini ili kuimarisha usimamizi wa shughuli za ufundishaji na ujifunzaji.
Hafla hii ya utiaji saini imefanyika leo Februari 2, 2026 ADEM Bagamoyo ambapo ushirikiano huu unatarajiwa kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi katika sekta ya elimu nchini ukihusisha kuwajengea uwezo viongozi wa elimu Mkoani Mara.





0 Comments