Ticker

6/recent/ticker-posts

Wawekezaji Wahimizwa Kuwekeza Viwanda vya Uchenjuaji Madini Singida

-Singida

Wawekezaji wa ndani na nje ya Mkoa wa Singida wamehimizwa kujitokeza kuwekeza katika viwanda vya uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini ili kunufaika na rasilimali zilizopo, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi.

Wito huo umetolewa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Sabai Nyansiri, akisema mkoa huo una fursa kubwa ya uwekezaji katika sekta ya madini kutokana na ongezeko la shughuli za uchimbaji na mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali.

Akizungumza wakati wa ziara yake kwa wachimbaji wadogo katika Mgodi wa Matongo uliopo Kata ya Ikungi, Wilaya ya Ikungi, Mhandisi Nyansiri amesema Singida inaendelea kufanya vizuri katika uchimbaji wa madini ya dhahabu, shaba, madini ya ujenzi pamoja na jasi, hivyo kuwepo kwa viwanda vya uchenjuaji ni hatua muhimu ya kuongeza thamani ya madini hayo kabla ya kuuzwa.

Amesema uwekezaji katika viwanda vya uongezaji thamani wa madini utaongeza ajira kwa vijana na wanawake, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo.

“Uwepo wa viwanda vya uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini utaongeza ajira, mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa kila mwananchi,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha masoko ya madini na kuendeleza biashara rasmi ya madini, akibainisha kuwa hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la mapato ya mkoa.

Ameeleza kuwa Mkoa wa Singida ulipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 30 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kutoka Shilingi Bilioni 24 mwaka wa fedha 2024/2025, na hadi kufikia Desemba 2025 tayari umefanikiwa kufikia asilimia 54 ya lengo hilo sawa na Shilingi Bilioni 16.

Mhandisi Nyansiri amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo wazawa.

Kwa upande wake, Meneja wa Mgodi wa Matongo, Japhet Madusa, ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa wachimbaji wadogo katika maendeleo ya sekta ya madini na kuiomba iendelee kuwawezesha kwa kuwapatia vitendea kazi vya kisasa pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha upatikanaji wa migodi.

Ameongeza kuwa mgodi huo unaendelea kushirikiana na jamii inayouzunguka kwa kutoa ajira kwa vijana wa eneo hilo, kuchangia vifaa vya ujenzi katika Shule ya Sekondari Matongo, Ofisi ya Kijiji cha Matongo pamoja na ujenzi wa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatua inayochangia maendeleo ya kijamii katika eneo hilo.

Post a Comment

0 Comments