Ticker

6/recent/ticker-posts

MAC PROMOTION YAZINDUA MBIO ZA MAC D MARATHON 2026 DAR

  Uongozi wa Mac Promotion umezindua rasmi mbio za Mac D Marathon 2026, zitakazofanyika Jumamosi, Julai 4, katika viwanja vya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), vilivyopo Kunduchi jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Serena Hotel, Mkurugenzi wa Mipango na Biashara wa kampuni hiyo, Denzel Deogratius Rweyunga, amesema mwaka huu wamejipanga kuleta mageuzi makubwa katika mbio za marathon nchini.

Amesema mbio hizo zitahusisha vipengele vya kilomita 5, 10 na 21 (Half Marathon), huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni “Go Green With Gas”, inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kulinda mazingira.

“Kama tunavyofahamu, nchi yetu kwa sasa inahamasisha matumizi ya nishati safi kwa kila Mtanzania. Sisi Mac Promotion tumeona tuungane na juhudi hizi za serikali kwa kuunga mkono kampeni hiyo,” amesema Denzel.

Ameongeza kuwa, ili kuwajumuisha watu wa rika zote, mwaka huu pia kutakuwa na mbio maalum za watoto za kilomita 2.

“Tumeanzisha mbio hizi za watoto ili kuwapa nafasi ya kushiriki michezo kwa ajili ya afya zao, huku wakishirikiana na wazazi wao. Tunataka siku hii iwe maalum kwa familia,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Denzel, waandaaji wamejipanga kuvutia washiriki wasiopungua 3,500 watakaoshiriki katika mbio hizo.

Washiriki wote watakaojisajili watapatiwa vifaa mbalimbali ikiwemo fulana, medali, namba za utambulisho (bib numbers), wristbands pamoja na mabegi ya mgongoni.

Amesema maandalizi yamekamilika kwa kiwango cha juu, ikiwemo uwepo wa vituo vya maji (water points), maji safi ya kunywa kutoka Kilimanjaro Natural Mineral Water, matunda, huduma ya kwanza pamoja na ulinzi na usalama wa washiriki kuanzia uwanjani hadi njiani.

Kwa wanaotaka kushiriki, usajili unafanyika kupitia tovuti ya www.macdmarathon.com , ambapo pia watapata maelezo yote muhimu ikiwemo maeneo ya kuchukulia vifaa.

Aidha, mbio hizo zitarushwa mubashara kupitia vituo vya ITV na East Africa Television.

Mbali na mashindano, Denzel amesema siku hiyo pia itakuwa ya burudani, ambapo kutakuwa na muziki wa moja kwa moja wa bendi ya FM Academia chini ya Patcho Mwamba, pamoja na nyama choma, michezo ya watoto na vinywaji mbalimbali.

Mac D Marathon 2026 inaandaliwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kilimanjaro Natural Mineral Water, Azania Bank, ITV, EB Maritime Group, Mart Group Ltd (Tanzanite Royal Gin na Tanzanite Crafted for Royalty), Kaluba, Radio One, EATV, Montage na Ayo TV.


Post a Comment

0 Comments