Dar es Salaam, 29 Mei 2026 — Bolt Tanzania jana iliwakutanisha wadhibiti, watunga sera, wawekezaji na viongozi wa sekta binafsi katika Bolt Tanzania Mobility Dialogue 2026, jukwaa la ngazi ya juu lililoandaliwa kwa ushirikiano na Mwananchi Communications, likilenga kujadili namna ya kujenga mifumo endelevu ya usafiri wa mtandao inayochochea maendeleo ya muda mrefu ya uchukuzi wa mijini.
Mjadala huo ulijikita katika athari za kanuni, mahusiano ya wawekezaji na ujumuishaji wa kiuchumi katika sekta ya usafiri, huku ukibainisha mchango wa moja kwa moja wa huduma za ride-hailing katika kukuza uchumi wa gig nchini.
Washiriki walisisitiza kuwa ride-hailing imekuwa sehemu muhimu ya uchumi wa mijini, ikisaidia safari za mwanzo na mwisho, kuongeza kipato kwa madereva na kukuza ujumuishaji wa kifedha kupitia mifumo ya kidijitali.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Meneja Mkuu Mwandamizi wa Bolt Afrika Mashariki, Dimmy Kanyankole, alieleza kuwa Tanzania imeibuka kuwa miongoni mwa masoko yanayokua kwa kasi zaidi kwa Bolt duniani.
Alibainisha kuwa maelfu ya madereva washirika nchini wanategemea aplikesheni hio kujipatia kipato, jambo linaloonesha nafasi ya sekta hiyo katika uchumi wa gig.
Katika hotuba yake kuu, Mkurugenzi wa Uchukuzi wa Barabara kutoka Wizara ya Uchukuzi, Andrew Magombana, alisisitiza kuwa mustakabali wa usafiri wa mijini unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wadhibiti, wawekezaji, watoa huduma wa teknolojia na jamii.
Alithibitisha dhamira ya Serikali kuimarisha viwango vya usalama, kuwezesha ubunifu unaowajibika, kuunganisha ride-hailing na mifumo ya kitaifa kama BRT na SGR, pamoja na kuhimiza suluhu rafiki kwa mazingira.
Mjadala huo pia ulirejea takwimu za Ripoti ya Uchumi wa Gig 2026 zinazoonesha kuwa ride-hailing inachangia takribani asilimia 2.8 ya Pato la Taifa nchini Afrika Kusini na dola bilioni moja kwa mwaka nchini Kenya.
Kwa mujibu wa Kanyankole, Bolt pekee nchini Tanzania inarejesha zaidi ya Shilingi bilioni moja kwa mwezi kama VAT kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikionesha fursa kubwa iliyopo iwapo uwekezaji utaendelea kuongezeka.
Bolt ilisisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wadau kuimarisha mfumo salama, jumuishi na unaovutia uwekezaji katika sekta ya usafiri nchini Tanzania.

0 Comments