
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Tume ya Taifa ya Mipango kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP leo Mei 22, imefanya mjadala uliyowakutanisha wadau wa maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia, watafiti na taasisi za elimu ya juu kujadili hatua mbalimbali na afua zinazoweza kutumika ili kukabiliana na athari za mgogoro wa ukanda wa Ghuba.
Akifungua mjadala huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti na za kimkakati ili kupunguza athari zinazotokana na mgogoro wa Ghuba kiuchumi na kwa wananchi.
Mhe. Mkumbo amesema hayo leo Mei, 22 jijini Dar es Salaam katika mjadala wa kitaalamu ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya Mipango kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa UNDP kwa lengo la kujadili athari, uhimilivu na fursa zinazotokana na mgogoro huo.
Akitaja hatua hizo, Prof. Mkumbo amesema kuwa ni pamoja na kufuatilia kwa karibu bei na upatikanaji wa mafuta, chakula, mbolea na usafiri, kulinda kaya zilizo katika mazingira hatarishi, kuimarisha akiba na usambazaji wa biadhaa muhimu.
“tutahakikisha wananchi wanaendelea kupata chakula cha kutosha na mbolea kwa bei himilivu, vile vile tutaendelea kufanya uthibiti wa gharama za nishati, ikiwa ni pamoja na kutumia fursa za maliasili tulizonazo kama Gesi asilia, madini, utalii na fursa ya miundombinu ya usafiri kuimarisha uchumi wa taifa” amesema Prof. Mkumbo.
Hatua hizo, zinalenga kukabiliana na athari kama vile kupanda kwa bei ya mafuta, usafirishaji na mbolea kunakoweza kuathiri maisha ya wananchi, uzalishaji na bajeti ya Serikali, hivyo Serikali itaendelea kuchukua hatua za haraka ili kuwalinda.
Aidha, Mheshimiwa Waziri ameeleza kuwa pamoja na changamoto hizo, mgogoro huo wa Ghuba unatoa fursa ya kipekee ya kiuchumi kwa Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla, hasa katika kuvutia uwekezaji mpya kwenye sekta ya nishati.
"Mgogoro huu unatoa mwanya mkubwa wa uwekezaji katika miundombinu ya mafuta, ikiwemo ujenzi wa viwanda vya kikanda vya kusafisha na kuchakata mafuta (regional refineries)," amesema Prof. Mkumbo.

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango Dkt. Tausi Kida alieleza kuwa mkutano huo unahusisha wadau wa maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia, watafiti na taasisi za elimu ya juu kujadili hatua mbalimbali na afua zinazoweza kutumika ili kukabilia na athari za mgogoro huo.
Majadiliano hayo yalihudhuriwa na Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa Bi. Susan Namondo na Mwakalishi Mkaazi wa Umoja wa Mtaifa, na Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania Bw. Shigeki Komatsubaram.






0 Comments