WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Bashiru Ally, amesema Tanzania na Italia zinaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo uchumi wa buluu, utalii, biashara, afya, elimu na utamaduni, hali inayochangia kukuza ustawi wa mataifa hayo mawili.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 80 ya Jamhuri ya Italia yaliyofanyika Dar es Salaam, Waziri Bashiru alisema Italia imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, hususan sekta ya utalii ambapo imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza shughuli za utalii visiwani Zanzibar.
Amesema Tanzania inathamini uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya mataifa hayo mawili na itaendelea kushirikiana na Italia katika kulinda na kuendeleza utamaduni, kuimarisha uchumi na kukabiliana kwa pamoja na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
“Tuko pamoja na taifa hili. Tunajivunia sana uhusiano uliopo kati ya mataifa haya mawili ambao umeendelea kuleta manufaa kwa wananchi wetu,” amesema Waziri Bashiru.
Kwa upande wake, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Seán Coppola, amesema maadhimisho hayo yanafanyika wakati ambapo Tanzania na Italia zinasherehekea miaka 65 ya mahusiano ya kidiplomasia yaliyowezesha kuimarika kwa ushirikiano katika nyanja za biashara, diplomasia ya uchumi, utamaduni na mazungumzo ya kisiasa.
Amesema katika kipindi cha mwaka uliopita, nchi hizo zimeendelea kupanua ushirikiano wake, huku biashara kati yao ikiongezeka kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa balozi huyo, mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Italia yaliongezeka kwa asilimia 210 kati ya mwaka 2024 na 2025.
Balozi Coppola amesema Italia pia inaendelea kusaidia maendeleo ya sekta ya kahawa nchini kupitia uhamishaji wa teknolojia na utaalamu wa kisasa unaolenga kuboresha mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Aidha, amesema nchi yake imeendelea kutoa mchango katika sekta ya afya, hususan katika huduma na uwezeshaji wa watu wenye ulemavu, akisisitiza kuwa maendeleo ya kiuchumi yanapaswa kuwa jumuishi na kuwafikia wananchi wote.
Akizungumzia mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, amesema Italia iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha maendeleo, amani na ustawi wa wananchi wake.
“Tunasherehekea miaka 80 ya Jamhuri ya Italia na miaka 65 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Italia na Tanzania. Urafiki wetu wa muda mrefu umeendelea kuwa msingi wa amani, maendeleo na ustawi wa mataifa yetu,” amesema.














0 Comments