Ticker

6/recent/ticker-posts

UHAMIAJI WA KAZI UWE DARAJA LA MAENDELEO, SI CHANZO CHA MATATIZO


UHAMIAJI wa kazi unaweza kuwa daraja la maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii badala ya chanzo cha mateso kwa wafanyakazi, iwapo utaongozwa na sera madhubuti na ushirikiano wa kikanda, Shirika la Kazi Duniani (ILO) limesema.

Akizungumza na waandishi wa habari Juni 10, 2026 jijini Dar es Salaam, Mshauri Mkuu wa Kiufundi kutoka ILO, Aida Awel, alisema uhamiaji ni sehemu ya uhalisia wa maisha ya jamii za kisasa na unaweza kuwa fursa kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ikiwa utasimamiwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Aida alisema usimamizi mzuri wa uhamiaji wa kazi unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya nchi za kikanda ili kuhakikisha wafanyakazi wahamiaji wanapata mazingira salama ya kufanya kazi na haki zao zinalindwa.

“Tanzania inayo nafasi ya kimkakati katika masuala ya uhamiaji wa kikanda. Uhamiaji ukiwa salama na wenye mpangilio unaweza kuleta manufaa makubwa kwa nchi za asili za wahamiaji pamoja na nchi zinazowapokea,” alisema.

Alieleza kuwa wafanyakazi wanapopata ajira zenye staha katika nchi wanazokwenda, hupata fursa ya kuchangia maendeleo ya familia zao na jamii kupitia fedha wanazotuma nyumbani, huku pia wakichangia ukuaji wa uchumi wa nchi husika.

Hata hivyo, alisema ili manufaa hayo yaweze kupatikana kwa kiwango kikubwa, ni muhimu kuwepo kwa mifumo imara ya kulinda haki za binadamu, sera na takwimu sahihi, pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zinazoshughulikia masuala ya uhamiaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jinsia, Wanawake na Vijana wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Mratibu wa Kituo cha Rasilimali kwa Wafanyakazi Wahamiaji, Nasra Shargy, alisema uhamiaji wa kazi unaendelea kuwa na umuhimu mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na mchango wake katika kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi.

Nasra alionya kuwa pamoja na fursa hizo, uhamiaji usio salama bado ni changamoto kubwa inayowaweka wafanyakazi katika hatari ya unyonyaji, matumizi mabaya, biashara ya binadamu na ukiukwaji wa haki za kazi.

Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi ili kuwasaidia kufanya maamuzi salama wanapotafuta ajira nje ya nchi.

Naye Mkuu wa Utafiti na Uhamasishaji Sera wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Renatus Mbamilo, alisema uhamiaji wa kazi ni suala linalohitaji mjadala mpana na utoaji wa taarifa unaozingatia ushahidi ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu fursa na changamoto zilizopo.

Mbamilo aliipongeza ILO kwa kuandaa jukwaa hilo ambalo limewakutanisha viongozi wa serikali, waajiri, wawakilishi wa wafanyakazi na waandishi wa habari kujadili namna bora ya kusimamia uhamiaji wa kazi kwa manufaa ya wafanyakazi, waajiri na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments