Ticker

6/recent/ticker-posts

UTEKELEZWAJI WA MIPANGO YA KUIMARISHA HAKI NA USTAWI KWA WATU WENYE ULEMAVU WASISITIZWA MWANZA

 

Na Mwandishi Wetu, Mwanza.

Serikali imezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa, watendaji wa sekta mbalimbali pamoja na wadau wa masuala ya Watu wenye Ulemavu kuhakikisha Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi kwa Watu wenye Ualbino (MTHUWWU) na Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi (NATS) vinatekelezwa kikamilifu ili kuboresha huduma na kulinda haki za Watu wenye Ulemavu nchini. 

Wito huo umetolewa leo Juni 26, 2026 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Kheri Kagya akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usambazaji na utoaji wa elimu kuhusu Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi kwa Watu wenye Ualbino pamoja na Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi kwa watendaji na wadau wenye ulemavu yaliyowakutanisha washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Mara na Geita katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Katika hotuba yake, Dkt. Kagya ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa sera na mipango inayolenga kuimarisha ustawi wa watu wenye ulemavu, akibainisha kuwa usambazaji wa nyaraka hizo utasaidia kuongeza uelewa kwa watendaji na viongozi wa SHIVYAWATA ili kuboresha utoaji wa huduma na kutokomeza ubaguzi, unyanyasaji na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino. 

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutekeleza hatua mbalimbali za kuboresha maisha ya Watu wenye Ulemavu, ikiwemo kuimarisha huduma za afya, elimu jumuishi, uwezeshaji wa kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri na asilimia 30 ya zabuni za manunuzi ya umma, pamoja na kuendeleza huduma za teknolojia saidizi. 

Ameongeza kuwa, pamoja na umuhimu mkubwa wa teknolojia saidizi katika kuwawezesha watu wenye ulemavu na wazee kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi, kiwango cha upatikanaji wa vifaa hivyo bado ni cha chini, hali inayolazimu wadau wote kushirikiana katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi wa mwaka 2024–2027. 

Pia, Dkt Kagya amewataka watendaji wa mikoa na halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa mafuta kinga kwa Watu wenye Ualbino na vifaa saidizi kwa Watu wenye Ulemavu, sambamba na kuhakikisha elimu iliyotolewa katika mafunzo hayo inawafikia watendaji wengine ili kuimarisha utoaji wa huduma jumuishi nchini. 

Awali, akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi, Afisa Sheria kutoka Kitengo cha Watu wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU) Bw. Jacob Mwinula, amesema usambazwaji na utoaji wa Elimu hiyo umeshafanyika katika mikoa mitano ambayo ni Mwanza, Geita, Mara, Manyara na Kilimanjaro pia amewaomba watendaji wote wa Halmashauri, Mikoa, Sekta mbalimbali na SHIVYAWATA kuhakikisha mikakati na shughuli zote zinazofanyika katika maeneo yao zinajumuisha utekelezaji wa mpango na mkakati huu na kufanya tathimini na ufuatiliaji ili kuimarisha maisha ya Watu wenye Ulemavu kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments