Ticker

6/recent/ticker-posts

DCEA YAKAMATA TANI 22.6 ZA DAWA ZA KULEVYA NDANI YA MIEZI MIWILI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata tani 22.6 za dawa za kulevya, lita 30.5 na kilogramu 19.94 za dawa tiba zenye asili ya kulevya katika operesheni zilizofanyika nchini kati ya Mei na Juni mwaka huu, huku watuhumiwa 188 wakitiwa mbaroni na mali mbalimbali zinazohusishwa na biashara hiyo zikikamatwa.

Katika operesheni hizo, DCEA pia ilikamata magari sita, bajaji mbili na pikipiki 33 zilizokuwa zikitumika katika usafirishaji wa dawa za kulevya. Aidha, iliteketeza ekari 228.5 za mashamba ya bangi pamoja na tani 3.3 za bangi na mirungi katika maeneo mbalimbali nchini.

Moja ya mafanikio makubwa ya operesheni hizo ni ukamataji wa kilogramu 19.94 za bidhaa zilizokuwa zikitambulishwa kama virutubisho vya lishe aina ya AFA CELL (Moringa Extract) katika eneo la mizigo ya kusafirishwa nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Uchunguzi wa maabara uliofanywa ulibaini kuwa bidhaa hizo, ambazo ziliingizwa nchini kutoka Malaysia na zilikuwa zikisafirishwa kwenda Barbados, zilikuwa na kiambata cha dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya Prazepam.

Kutokana na tukio hilo, Agustino Metusela Ismaely (30), mkazi wa Kimara; Zamia Harid Upunda (23), mkazi wa Bungoni, Ilala; na Habiba Ally Mziga (54), mkazi wa Mbezi Makonde walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

DCEA imeeleza kuwa Prazepam ni dawa inayotumika kutibu magonjwa mbalimbali ikiwemo wasiwasi, msongo wa mawazo na kukosa usingizi, lakini matumizi yake bila usimamizi wa daktari yanaweza kusababisha uraibu, kuathiri mfumo wa fahamu na wa upumuaji, kupoteza fahamu na hata kifo.

Katika operesheni nyingine iliyofanyika eneo la Manyanya, Kinondoni, zilikamatwa kilogramu 34.87 za mirungi zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Tarakea, mkoani Kilimanjaro, baada ya kuingizwa nchini kutoka Kenya.

Mirungi hiyo ilikuwa imefichwa kwa kuchanganywa na matenga ya nyanya ili kuficha uhalisia wa mzigo kabla ya kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kwa kutumia bajaji.

Watuhumiwa Mohamed Omary Mohamed (24), Suleman Omary Suguti (34) na Deo Paschal Maratua (32) walikamatwa, huku Husseni Jumaa Salimu (52), anayedaiwa kuwa nchini Kenya, akiendelea kusakwa.

Katika hatua nyingine, operesheni ya pamoja iliyoshirikisha DCEA, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ilibaini vinywaji aina ya TRIP Energy Drink vyenye kemikali ya THC, kiambata kinachopatikana kwenye bangi.

Jumla ya makopo 122 yenye ujazo wa mililita 250 kila moja, sawa na lita 30.5, yalikamatwa katika duka la Village Supermarket jijini Dar es Salaam. Watuhumiwa Syed Abdul Bast (43), raia wa Pakistan, na Dhirendra Kumar Gorodhan (45), Mtanzania mwenye asili ya Asia, walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Kwa mujibu wa DCEA, THC huathiri mfumo wa fahamu, inaweza kuamsha magonjwa ya akili na kuchochea vitendo vya uhalifu pamoja na matumizi ya dawa nyingine za kulevya.

Operesheni nyingine zilizofanyika katika Bandari ndogo ya usafiri wa boti kati ya Dar es Salaam na Zanzibar zilisababisha kukamatwa kwa gramu 972.05 za mirungi na mtuhumiwa Kalsam Abdurahman Sebbi (43), raia wa Kenya. Wilayani Kigamboni, gramu 162.48 za heroin zilikamatwa huku mtuhumiwa Omary Miraji Mbonaeni akitiwa mbaroni.

Mkoani Arusha, DCEA ilikamata kilogramu 106.04 za mirungi zilizokuwa zikisafirishwa kwa gari aina ya Toyota Premio, huku mtuhumiwa Goodluck Erasto Nyakaselula (35), ambaye ni mtaalamu wa picha za kitabibu katika Hospitali ya Ocean Road, akikamatwa.

Wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, kilogramu 240 za mirungi zilizokuwa zimefichwa ndani ya mabegi ya nguo zilikamatwa na watuhumiwa Irene Obedi Sule pamoja na Eliasi Obedi Sule kutiwa mbaroni.

Katika mikoa mingine nchini, operesheni hizo zilisababisha kukamatwa kwa tani 19.5 za bangi, tani 2.6 za mirungi, kilogramu 40 za skanka na gramu 11.63 za heroin. DCEA pia iliteketeza tani 3.3 za bangi na mirungi pamoja na ekari 228.5 za mashamba ya bangi katika wilaya za Chamwino, Kilwa, Sengerema na Geita.

Wakati huohuo, DCEA imesema imebaini baadhi ya raia wa Tanzania wanaohusishwa na mitandao ya kimataifa ya biashara ya dawa za kulevya waliokimbilia nchini Eswatini, Afrika Kusini, Msumbiji na Zambia.

Mamlaka hiyo imesema itaendelea kushirikiana na vyombo vya usalama vya nchi hizo kuwakamata watuhumiwa hao, huku ikiimarisha ushirikiano na taasisi za udhibiti nchini katika kukabiliana na mbinu mpya za usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia virutubisho vya chakula, dawa na kemikali.

Post a Comment

0 Comments