NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WANANCHI wanaotembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) mwaka huu watapata fursa ya kujionea kwa mara ya kwanza sampuli za aina mbalimbali za dawa za kulevya pamoja na kemikali zinazotumika kuzitengeneza kupitia mabanda ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu madhara ya matumizi na biashara haramu ya dawa hizo.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa wa DCEA, Shaban Miraji, amesema mamlaka hiyo imeandaa mabanda mawili kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi, likiwemo moja lililotembelewa na Waziri Mkuu na lingine lililopo katika eneo la Serikali.
Amesema katika kipindi chote cha maonesho, wananchi watapata nafasi ya kujifunza kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, athari za biashara haramu ya dawa hizo pamoja na wajibu wa kila mmoja katika kushiriki mapambano dhidi ya tatizo hilo.
"Tunawaalika wananchi wote watakaofika Sabasaba kutembelea mabanda yetu ili wapate elimu sahihi kuhusu dawa za kulevya na madhara yake. Hii ni fursa muhimu kwa jamii kujifunza na kuongeza uelewa," amesema Miraji.
Amefafanua kuwa moja ya vivutio vikubwa katika mabanda hayo ni maonesho ya sampuli za dawa mbalimbali za kulevya, zikiwemo bangi, heroini na kemikali zinazotumika katika utengenezaji wa dawa hizo.
"Kuna watu wengi husikia majina ya dawa za kulevya lakini hawajawahi kuziona. Wapo hata wazazi ambao watoto wao wanatumia dawa hizo lakini hawazitambui. Tunawapa wananchi nafasi ya kuziona kwa macho ili waweze kuzitambua na kuchukua hatua mapema wanapokutana nazo," amesema.
Mbali na maonesho ya sampuli za dawa hizo, Miraji amesema wananchi watapata machapisho mbalimbali ya elimu, majarida na nakala za sheria zinazohusu udhibiti wa dawa za kulevya, huku wataalamu wa DCEA na wanasheria wakitoa ufafanuzi na kujibu maswali yote yanayohusu matumizi, athari na biashara haramu ya dawa hizo.
Aidha, amesema kampeni hiyo inalenga zaidi kuwafikia vijana, ambao ni kundi linaloathirika kwa kiwango kikubwa na matumizi ya dawa za kulevya kutokana na kukosa taarifa na elimu sahihi kuhusu madhara yake.
Amesema elimu inayotolewa katika maonesho hayo inalenga kuwajengea vijana uelewa utakaowasaidia kufanya maamuzi sahihi, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kuwa mabalozi wa kuelimisha wenzao na jamii kuhusu athari za tatizo hilo.
"Vijana wakipata elimu sahihi wanakuwa sehemu ya suluhisho. Tunataka waondoke hapa wakiwa na maarifa ya kujilinda na uwezo wa kuelimisha wengine ili kwa pamoja tuendelee kupunguza tatizo la dawa za kulevya nchini," amesema Miraji.





0 Comments