Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, ameipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa juhudi zake za kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia Kituo chake cha Kiatamizi cha IAA Business Start Up Centre, kinachowasaidia kubadili mawazo ya kibunifu kuwa biashara zenye mafanikio.
Tutuba alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la IAA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Alisema anafurahishwa na maendeleo ya kituo hicho, akieleza kuwa anakumbuka hatua za mwanzo za kuanzishwa kwake na sasa anashuhudia matokeo chanya kupitia vijana wanaobuni na kuanzisha biashara zinazochangia maendeleo ya uchumi.
"Ninakumbuka tulipoanzisha kituo hiki. Leo ninafurahi kuona kinaendelea kuzalisha vijana wenye ubunifu na kuwageuza mawazo yao kuwa fursa za kiuchumi," alisema Tutuba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa, Uhusiano na Masoko wa IAA, Sarah Goroi, alisema taasisi hiyo imeendelea kuwekeza katika kuwaandaa vijana kwa kujiajiri kupitia Kituo cha Kiatamizi, sambamba na kutoa elimu inayokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Alisema mbali na mafunzo ya darasani, IAA imeweka mazingira rafiki yanayowezesha wanafunzi kuanzisha biashara zao huku wakipata ushauri wa kitaalamu, mafunzo ya ujasiriamali na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha mawazo yao yanakua na kuwa biashara endelevu.
Sarah alisema katika mwaka wa masomo 2024/2025 zaidi ya vijana 8,600 walinufaika na programu za ujasiriamali, huku vijana 1,520 wakiwasilisha mawazo mbalimbali ya biashara kupitia kituo hicho.
Aliongeza kuwa kati ya mawazo hayo, zaidi ya biashara 50 zilianzishwa na kampuni 12 zikafanikiwa kusajiliwa rasmi, zikijikita katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, teknolojia, sanaa, uhifadhi wa mazingira na shughuli nyingine za kiuchumi.
Alisema kupitia Kituo cha Kiatamizi, wahitimu wengi wamefanikiwa kujiajiri na wengine kuanzisha kampuni zinazowaajiri vijana wenzao, hatua inayochangia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia ubunifu na ujasiriamali.





0 Comments