Ticker

6/recent/ticker-posts

MKENDA: MIAKA 40 YA COSTECH ISIWE YA SHEREHE, IWE YA TAFAKURI

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameutaka uongozi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kufanya tathmini ya kina ya mchango wake katika kipindi cha miaka 40 iliyopita badala ya kujikita katika kusherehekea mafanikio.

Profesa Mkenda alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (NISST) pamoja na uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya miaka 40 ya COSTECH.

Alisema maadhimisho hayo yanapaswa kuwa fursa ya kutafakari kwa uhalisia namna sayansi, teknolojia na ubunifu vilivyochangia kuboresha maisha ya Watanzania na kuchochea maendeleo ya taifa.

"Tunapoadhimisha miaka 40 ya COSTECH, lazima tujiulize tumewasaidia wananchi kwa kiwango gani. Je, tumesaidia kuwaondoa katika umaskini? Tumeitumia kwa kiasi gani sayansi na teknolojia kuongeza tija katika kilimo?" alihoji.

Alisisitiza kuwa viongozi na watendaji wa COSTECH wanapaswa kuwa wakweli kwa nafsi zao na kwa taifa katika kutathmini kama wamefanikiwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi katika kipindi cha miongo minne iliyopita.

Profesa Mkenda alisema maadhimisho hayo yanapaswa pia kuwa sehemu ya mapitio ya Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ili iendane na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alieleza kuwa sayansi, teknolojia na ubunifu havipaswi kubaki katika maabara au kuishia kwenye maonesho, bali vinapaswa kutoa suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta muhimu kama kilimo, afya, viwanda na uchumi.

Aidha, alisisitiza kuwa tafiti za kisayansi zinapaswa kuongeza tija ya uzalishaji, kuinua mavuno ya wakulima na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

"Matokeo ya utafiti yanapaswa kuonekana sokoni na katika maisha ya wananchi, si kubaki kuwa kaulimbiu au maonesho ya muda," alisema.

Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda alizitaka taasisi za utafiti kufanya uchunguzi wa kisayansi wa tiba za asili kupitia majaribio ya awali na ya kitabibu ili kuthibitisha ufanisi wake, na pale zitakapothibitika zigeuzwe kuwa bidhaa rasmi za dawa, huku zisizothibitika zikitolewa ufafanuzi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo alisema maadhimisho ya miaka 40 ya COSTECH yanatoa nafasi ya kutafakari historia ya uwekezaji wa Serikali katika sayansi, teknolojia na ubunifu pamoja na mchango wake katika kutatua changamoto za jamii.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu alisema Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (NISST) umeunganisha huduma mbalimbali za taasisi hiyo katika jukwaa moja.

Alifafanua kuwa mfumo huo utasimamia shughuli za tafiti, ubunifu, usajili wa watafiti, ufadhili wa tafiti pamoja na huduma nyingine, huku ukiwezesha taifa kuwa na taarifa sahihi za watafiti, maeneo yao ya kazi na maendeleo ya ubunifu kwa wakati halisi.

Dk. Nungu alisema mfumo huo pia utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali, ikiwemo wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, hatua ambayo itarahisisha uratibu wa shughuli za utafiti na ubunifu nchini.

Post a Comment

0 Comments