
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi na uhamisho wa Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa, katika mabadiliko yanayogusa mikoa kadhaa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Leo Agosti 27,2026 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, mabadiliko hayo yamefanyika kwa uteuzi na uhamisho wa baadhi ya viongozi, huku wengine wakiachiwa nafasi zao kutokana na kustaafu au kupangiwa majukumu mengine.
WAKUU WA MIKOA
Katika uteuzi huo, CP Salum Rashid Hamduni, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, amehamishiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Aidha, Bw. Alexander Pastory Mnyeti ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Bw. Stanlaus Haroon Nyongo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, na Bw. Jumanne Abdallah Sagini kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Kwa upande wa uhamisho, Mhe. Martine Reuben Shigela amehamishwa kutoka Geita kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Mhe. Said Mohamed Mtanda amehamishwa kutoka Mwanza kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, akichukua nafasi ya Bw. Anamringi Macha, ambaye ameacha nafasi hiyo kutokana na kustaafu.
Vilevile, Mhe. Abubakar Mussa Kunenge amehamishwa kutoka Pwani kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, akichukua nafasi ya Bw. Jabiri Omari Makame, ambaye atapangiwa majukumu mengine.
Mhe. Beno Moris Malisa amehamishwa kutoka Mbeya kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, akichukua nafasi ya Mhe. Paul Matiko Chacha, ambaye ameteuliwa kuwa Katibu wa NEC, Idara ya Oganaizesheni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, Mhe. Adam Kighoma Malima amehamishwa kutoka Morogoro kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, akichukua nafasi ya Bi. Zainab Telack, ambaye amestaafu.
Mhe. Queen Cuthbert Sendiga naye amehamishwa kutoka Manyara kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
MABADILIKO YA MAKATIBU TAWALA
Kwa upande wa Makatibu Tawala wa Mikoa, Bw. Richard Marcellino Kayombo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani.
Bw. Balandya Mayuganya Elikana amehamishwa kutoka Mwanza kwenda Mbeya, huku Dkt. Fatuma Ramadhan Mganga akihamishwa kutoka Singida kwenda Mwanza.
Aidha, Bi. Pili Hassan Mnyema amehamishwa kutoka Pwani kwenda kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga.
Bw. Rodrick Lazaro Mpogolo naye amehamishwa kutoka Mbeya kwenda kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida.
Taarifa hiyo imesema uapisho wa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wateule utafanyika kwa tarehe itakayopangwa baadaye.
Mabadiliko hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mamlaka ya Rais katika kupanga na kuimarisha uongozi wa Serikali katika ngazi za mikoa.



0 Comments