Ticker

6/recent/ticker-posts

BOT YAWATAKA WASANII KUWA MABALOZI WA ELIMU YA FEDHA

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wasanii na wadau wengine wenye ushawishi kwa jamii kuwa mabalozi wa elimu ya matumizi sahihi ya fedha, ikiwemo umuhimu wa kutunza noti na sarafu kwa usahihi.

Akizungumza leo, Agosti, 31 2026 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti na Uchumi wa BoT, Dk. Suleiman Misango, amesema hayo wakati wa semina iliyowakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu matumizi na utunzaji bora wa fedha zinazotolewa na benki hiyo.

Amesema BoT imeamua kuwashirikisha wadau hao kwa sababu wana uwezo mkubwa wa kufikisha elimu ya fedha kwa wananchi kupitia majukwaa yao na shughuli mbalimbali wanazofanya katika jamii.

“Tumekuwa tukifanya kazi hii kwenye maonesho na matukio mbalimbali, lakini tumeona wadau hawa wanaweza kutusaidia kufikisha elimu kwa jamii kwa njia bora zaidi,” amesema Dkt. Misango.

Ameeleza kuwa utunzaji mzuri wa noti na sarafu unaweza kusaidia kupunguza gharama zinazotumika kuchapisha na kusambaza fedha mpya, ambazo hulazimika kuingizwa kwenye mzunguko baada ya zile zilizopo kuchakaa au kuharibika.

Dkt. Misango pia ametoa wito kwa wananchi kubadili baadhi ya desturi za kutoa fedha taslimu katika sherehe, akisema kwa zawadi kubwa za fedha, mtu anaweza kuweka fedha hizo moja kwa moja kwenye akaunti ya anayempa zawadi badala ya kubeba kiasi kikubwa cha fedha taslimu.

Amesema noti na sarafu za Tanzania ni miongoni mwa alama za utaifa na mamlaka ya nchi, hivyo zinapaswa kuheshimiwa na kutunzwa kama ilivyo kwa alama nyingine za taifa.

Kwa upande wake, Afisa wa BoT kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Joseph Lubava, amewataka wananchi na wasanii wanaotaka kuanzisha au kujiunga na huduma za fedha kuhakikisha wanafuata taratibu za kisheria na kushirikiana na taasisi zenye leseni.

Lubava amesema sheria ya huduma ndogo za fedha imeweka madaraja mbalimbali ya huduma hizo, ikiwemo benki za huduma ndogo za fedha, SACCOS, vikundi vya huduma ndogo za fedha pamoja na watoa huduma za mikopo, huku kila kundi likiwa na taratibu zake za usajili na usimamizi.

Amesisitiza kuwa mtu anayehitaji mkopo anapaswa kwanza kuhakiki kama taasisi anayokwenda kukopa ina leseni halali kutoka BoT, kisha asome kwa makini mkataba wa mkopo, ikiwemo riba, tozo, gharama nyingine na masharti ya urejeshaji.

Aidha, Lubava amewataka wasanii kutumia umaarufu wao kuelimisha jamii badala ya kuitumia kueneza taarifa zinazoweza kupotosha wananchi kuhusu huduma za fedha, akisema mtu maarufu ana uwezo wa kufikisha ujumbe kwa watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi.

Amesema wananchi wanaweza kupata taarifa na kuwasilisha malalamiko kuhusu huduma za kifedha kupitia mifumo na dawati la malalamiko la Benki Kuu, huku akiwashauri kufikisha malalamiko mapema kabla hawajaingia katika mikataba yenye masharti wasiyoyaelewa.

Post a Comment

0 Comments