
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Meja Edward Gowele, amewataka wananchi wa Kijiji cha Nyangoto, Kata za Mangoto na Nyangoto, kusitisha mara moja uendelezaji maeneo yanayoguswa na Mradi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na Barrick, wakati Serikali ikiendelea na hatua za uthamini.
Katazo hilo limetolewa katika kikao cha uhamasishaji kilichofanyika Agosti 24, 2026 katika Vijiji vya Matongo na Nyangoto, Kata ya Matongo wilayani Tarime mkoa wa Mara kilichowakutanisha wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wawakilishi wa Haki za Binadamu, Kamati ya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Halmashauri pamoja na wananchi wanaoguswa na mradi wa ujenzi wa Bwawa la TSF.
Mradi huo unatarajiwa kuchukua takribani ekari 420, hivyo Serikali imeanza kusimamia zoezi la uthamini ili kuhakikisha wananchi wanaostahili wanapata fidia kwa kuzingatia sheria, haki na usawa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Gowele amewataka wataalamu wanaosimamia zoezi la uthamini kutenda haki, kuwa waaminifu na kuhakikisha hakuna udanganyifu wowote unaofanyika.
“Inawezekana mtu asiwe na eneo katika eneo la mradi na akaamua kufanya ujanja wa kujiweka ili apate fidia. Kufanya hivyo ni kujiingiza matatizoni na hatutafumbia macho jambo hilo,” amesema.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amekemea vikali vitendo vya kutengeneza mikataba bandia au kuwasilisha taarifa zisizo sahihi kwa lengo la kujipatia fidia na kuwataka wananchi, viongozi na wadau kuhakikisha mchakato huo unaendeshwa kwa uwazi.
“Isitokee kutengenezwa mikataba 'fake', tusione migogoro isiyo na kina. Tuache watu wapate haki yao stahiki na viongozi wasishiriki katika dhulma,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa, katazo hilo linazingatia masharti ya sheria za ardhi na kuwataka wananchi kutoanzisha ujenzi, kubadilisha matumizi ya ardhi au kufanya uendelezaji mpya katika maeneo yanayoguswa na mradi bila kufuata taratibu za kisheria.
Kikao hicho ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha zoezi la uthamini na ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaoguswa na mradi wa North Mara linafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia sheria.







0 Comments