Kaimu Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Bi. Nasieku Kisambu, akizungumza na Wathamini na Wataalamu wanaoshiriki katika zoezi la uthamini wa mali za wananchi wanaotarajiwa kuhamishwa kupisha ujenzi wa eneo jipya la kuhifadhia mabaki ya shughuli za uchimbaji madini (Tailings Storage Facility – TSF) katika Kijiji cha Matongo, Wilaya ya Tarime.
Kaimu Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Bi. Nasieku Kisambu, akizungumza na Wathamini na Wataalamu wanaoshiriki katika zoezi la uthamini wa mali za wananchi wanaotarajiwa kuhamishwa kupisha ujenzi wa eneo jipya la kuhifadhia mabaki ya shughuli za uchimbaji madini (Tailings Storage Facility – TSF) katika Kijiji cha Matongo, Wilaya ya Tarime.
Afisa Mwandamizi wa Usalama Mahali pa Kazi, Bw. Francisco Michael Ntemi, akizungumza na Wathamini pamoja na wataalamu wanaoshiriki katika zoezi la uthamini wa mali za wananchi katika Kijiji cha Matongo, Wilaya ya Tarime. Bw. Ntemi amewataka wataalamu hao kutambua vihatarishi (hazards), kutathmini hatari (risks) na kuchukua hatua stahiki za udhibiti ili kuhakikisha usalama wao na wa jamii wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.
Mthamini Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali, Bw. Baraka Mollel, akizungumza na Wataalamu na Wathamini wanaoshiriki katika zoezi la uthamini wa mali za wananchi katika Kijiji cha Matongo, Wilaya ya Tarime.
Bw. Mollel amewasisitiza wataalamu hao kutoa taarifa mara moja wanapobaini vitendo vya hatari au uvunjifu wa amani, huku akiwataka kuzingatia sheria na taratibu wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.
***
Wataalamu wanaoshiriki katika zoezi la uthamini wa mali za wananchi wanaotarajiwa kuhamishwa kupisha ujenzi wa eneo jipya la kuhifadhia mabaki ya shughuli za uchimbaji madini (Tailings Storage Facility – TSF) katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, wamehimizwa kuzingatia kikamilifu taratibu za usalama wanapokuwa katika maeneo ya kazi.
Hayo yamesemwa Hivi karibuni na Afisa Mwandamizi wa Usalama Mahali pa Kazi, Bw. Francisco Michael Ntemi, wakati akizungumza na Wathamini pamoja na wataalamu wengine wanaoshiriki katika zoezi hilo katika Kijiji cha Matongo, Wilaya ya Tarime.
Bw. Ntemi amewataka wataalamu hao kuwa na utamaduni wa kutanguliza usalama kwa kuhakikisha wanatambua mapema vihatarishi (hazards) vinavyoweza kujitokeza katika maeneo yao ya kazi, kutathmini hatari (risks) zinazoweza kusababishwa na vihatarishi hivyo na kuchukua hatua stahiki za udhibiti kabla na wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, amewasisitiza wataalamu hao kutofanya kazi kwa mazoea, bali kuwa makini na mazingira yanayowazunguka, kutumia vifaa stahiki vya kujikinga (Personal Protective Equipment – PPE) pale inapohitajika, pamoja na kutoa taarifa mapema kuhusu mazingira au vitendo visivyo salama.
“Kila mnapokuwa sehemu za kazi, hakikisheni mnatambua vihatarishi vilivyopo, mnatathmini hatari zinazoweza kujitokeza na kuchukua hatua stahiki za kudhibiti hatari hizo kabla ya kuendelea na kazi. Usalama unatakiwa kuwa sehemu ya kila hatua mnayochukua,” amesema Bw. Ntemi.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mahusiano Mgodi wa Barrick North Mara, Bi. Nasieku Kisambu, amewataka wataalamu hao kuwa mstari wa mbele katika kuzingatia masuala ya usalama wakati wote wanapotekeleza majukumu yao katika maeneo yanayohusika na mradi huo.
Naye Mthamini Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali, Bw. Baraka Mollel, amewasisitiza wataalamu hao kutoa taarifa mara moja pale wanapobaini vitendo au mazingira yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama, huku akiwataka kuendelea kuzingatia sheria, taratibu na miongozo inayosimamia utekelezaji wa majukumu yao.
Zoezi la uthamini wa mali linaendelea katika Vijiji vya Matongo na Nyangoto, Wilaya ya Tarime, likilenga kubaini na kuthamini mali za wananchi wanaotarajiwa kuhamishwa ili kupisha ujenzi wa eneo jipya la kuhifadhia mabaki ya shughuli za uchimbaji madini (TSF) katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.













0 Comments