Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS DKT.MPANGO AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI WA DORIS MOLLEL FOUNDATION


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation inayojihusisha na kusaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) Bi. Doris William Mollel, Mazungumzo yaliofanyika Jijini Dar es salaam leo tarehe 25 Julai 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation inayojihusisha na kusaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) Bi. Doris William Mollel, mara baada ya Mazungumzo yaliofanyika Jijini Dar es salaam leo tarehe 25 Julai 2022.

*************************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 25 Julai 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation inayojihusisha na kusaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) Bi. Doris William Mollel, Mazungumzo yaliofanyika Jijini Dar es salaam.

Makamu wa Rais amempongeza mkurugenzi huyo kwa jitihada anazofanya katika kuchangia vifaa tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwaajili ya kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti). Amesema taasisi hiyo inapaswa kuwekeza pia katika utoaji elimu ya afya ya uzazi ili kukabiliana na ongezeko la Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwani maeneo mengi hasa ya vijijini wanashindwa kupata uelewa juu jambo hilo.

Makamu wa Rais amesema serikali imeendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa ujenzi wa hospitali za wilaya, vituo vya afya katika kata pamoja na zahanati katika vijiji ili kuendelea kukabiliana na changamoto za vifo vya mama na mtoto. Ametoa wito kwa wadau, taasisi za dini pamoja na wananchi kwa ujumla kulipa kipaumbele suala la kuwasaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ili kukabiliana na changamoto ya vifo vinavyotokana na hali hiyo.

Katika Mazungumzo hayo Bi. Doris Mollel amempongeza Makamu wa Rais kwa jitihada alizofanya za kutambua changamoto zinazojitokeza katika malezi ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati hapa nchini na kuamua kuchangia vifaa tiba kwaajili ya watoto hao katika hospitali ya taifa Muhimbili hivi karibuni. Aidha ameishukuru serikali kwa kuendelea kuiunga mkono taasisi hiyo husasani katika ajenda ya mtoto njiti na tayari wamewasilisha ombi la kuongezwa likizo kwa wanaojifungua kabla ya wakati pamoja na kuwasilisha maoni ya kuwekwa elimu ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati katika masomo ya sayansi kwa shule za msingi na baiolojia kwa shule za sekondari.


Amesema tayari serikali imetenga shilingi bilioni 23.36 katika bajeti ya Wizara ya afya kwa mwaka 2022/2023 pamoja na kutenga vyumba mia moja kwaajili ya watoto njiti ili kuweza kupunguza idadi ya watoto njiti wanaopoteza maisha kutokana na changamoto mbalimbali. Ameongeza kwamba taasisi hiyo ibeba ajenda ambayo imeridhiwa ya kuhakikisha huduma za mtoto njiti zinawekwa katika bima ya afya ya mama wa mtoto ili kuepusha gharama kubwa zinazojitokeza wakati wa kumhudumia mtoto anapozaliwa kabla ya wakati.

Post a Comment

0 Comments