Matinyi, akisalimiana na Waziri wa Biashara ya Kimataifa wa Algeria, Mhe. Kamel Rezig, wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Biashara ya Afrika jijini Algiers, mwishoni mwa wiki.

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, akipatiwa maelezo ya namna kampuni ya Riad Hanieth Food Supplies ya Jordan yenye tawi lake nchini Tanzania inavyouza bidhaa za Tanzania katika soko la dunia kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wake, Riad Hanieth. Kulia ni Meneja wa Uzambazaji, Mira Hanieth.

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, akipata maelezo kutoka kwa Abdelkader Hamdi Mansour, Mshauri na Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya GETEX inayomilikiwa na Serikali ya Algeria. Kulia ni Hgersa Yahia, Mkurugenzi Mkuu wa ACED, kampuni tanzu ya bidhaa za ngozi ya GETEX.
****
Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki kwenye Maonesho ya 57 ya Kimataifa ya Biashara ya Algiers (FIA) yatakayofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 27 Juni, 2026, jijini Algiers, na kushirikisha kampuni takribani 700 kutoka nchi zaidi ya 40 duniani.
Balozi Matinyi alitoa wito huo baada ya kutembelea Maonesho ya Biashara ya Afrika yaliyofunguliwa tarehe 6 Juni, 2026, jijini Algiers na Waziri wa Biashara ya Kimataifa wa Algeria, Mhe. Kamel Rezig, na kushirikisha kampuni za Algeria na nchi 27 za Afrika.
Balozi Matinyi alisema maonesho hayo yanayokuja yanaandaliwa na taasisi ya serikali iitwayo Kampuni ya Maonesho na Biashara ya Nje ya Algeria (SAFEX), na yatakuwa makubwa zaidi na yatatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania watakaokuja kama washiriki au wageni kupata masoko mapya, ubia, ubunifu, maarifa na kusaini mikataba ya kibiashara katika sekta za kilimo na ufugaji, viwanda, madini, nishati, usafirishaji, ujenzi, utalii, fedha na huduma.
Kati ya kampuni zilioonesha bidhaa zake kwenye maonesho yanayoendelea sasa ya Afrika ilikuwa kampuni ya Jordan ya Riad Hanieh Food Supplies yenye tawi lake nchini Tanzania. Kampuni hii huuza mazao ya kilimo ya Tanzania pekee kama kahawa, korosho, karafuu, viungo na vanila kwenye soko la kimataifa.
Balozi Matinyi pia alifanya mazungumzo na uongozi wa kampuni ya GETEX inayomilikiwa na Serikali ya Algeria na kukubaliana kwamba ifanye ziara nchini Tanzania ili kutafuta ngozi na kuangalia uwezekano wa kufungua kiwanda cha kuchakata ngozi kwa ajili ya viwanda vyake nchini Algeria.
“Tutakwenda Tanzania kutafuta ngozi na kuangalia uwezekano wa kufungua kiwanda cha kuchakata ngozi huko Tanzania kwa ajili ya viwanda vyetu hapa Algeria”, alisema Abdelkader Hamdi Mansour, Mshauri na Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa GETEX. Katika mazungumzo hayo na Balozi Matinyi alikuwepo pia Ghersa Yahia, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni yao tanzu ya bidhaa za ngozi.
Balozi Matinyi alifafanua kwamba wafanyabiashara na wageni kutoka Tanzania watakaotaka kuja Algiers kwenye maonesho hayo wanaweza kupata maelezo ya kina kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria, Ubalozi wa Algeria nchini Tanzania, Mamlaka ya Maendeleo Biashara Tanzania (TanTrade) au Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania,
Algiers, Juni 7, 2026.

0 Comments