Ticker

6/recent/ticker-posts

WASUSI KUTOA ELIMU YA NISHATI SAFI, ORYX GAS NA KIDOTI FOUNDATION WATIA SAINI MAKUBALIANO

Na Mwandishi Wetu 

KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania kwa kushirikana na taasisi ya Kidodi Foundation wameingia makubaliano ya kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini kwa kulifiki kundi la watoa huduma za Saluni nchini.

Kwa mujibu wa Oryx na Kidodi Foundation watoa huduma za Saluni nchini ni kundi lenye uwezo mkubwa wa kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutokana na mwingiliano wao wa karibu na jamii, hali inayowafanya kuwa mabalozi muhimu wa mabadiliko ya tabia na mtazamo kuhusu matumizi ya nishati hiyo.

Akizungumza leo Juni 26,2026 Jijini Dar es Salaam wakakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo Mkurugenzi wa Kidoti Foundation, Jokate Mwegelo, ambaye pia ni mlezi wa Chama cha Salunisti Tanzania (CCST) amesema lengo la kuwawezesha watoa huduma za saluni kutumia nishati safi na kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi yake katika jamii.

Amesema kundi la wasusi na watoa huduma za saluni lina nafasi ya kipekee kwa kuwa hukutana na mamia ya wananchi kila siku, jambo linaloweza kutumiwa kueneza elimu kuhusu manufaa ya nishati safi ya kupikia kwa urahisi kuliko kutegemea kampeni za kawaida pekee.

Amefafanua watoa huduma za saluni wanazungumza na watu wa makundi mbalimbali kila siku. Wanajenga mahusiano ya karibu na wateja wao, hivyo wana nafasi kubwa ya kubadilisha mitazamo kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia. 

“Tunataka wawe mabalozi wa mabadiliko hayo na kupitia makubaliano haya tumeyaingia Kati ya Kidoti Foundation na Oryx Gas Tanzania matarajio yetu tutawafikia watoa huduma wote wa saluni kupitia chama chao ambapo tutawapatia mitungi ya gesi na tutaanza na mitungi 2000 ambayo itatolewa kwa awamu.

“Juhudi za kuhakikisha Watanzania wengi wanatumia nishati safi haziwezi kuachiwa Serikali pekee, bali zinahitaji ushiriki wa makundi yenye ushawishi wa moja kwa moja katika jamii.

Kundi la watoa huduma za saluni limesahaulika kwa muda mrefu lakini Kidoti Foundation tumeona iko haja ya kulishika kundi hili kwa kuliwezesha kutumia nishati safi ya kupikia.”

Jokate amesema saluni zimekuwa sehemu ambazo mbali na huduma za urembo, wananchi hubadilishana uzoefu kuhusu afya, biashara, malezi na masuala mbalimbali ya maendeleo, hivyo zinaweza pia kuwa majukwaa ya utoaji wa elimu kuhusu nishati safi.

Pia amesema kupitia ushirikiano huo, watoa huduma za saluni watanufaika kwa kutumia nishati safi katika shughuli zao za kila siku, huku wakipata nafasi ya kuwahamasisha wateja wao kuachana na matumizi ya nishati zinazochafua mazingira na kuhatarisha afya.

"Nishati safi si suala la kupikia pekee. Ni suala la afya, mazingira, uchumi wa familia na maendeleo ya taifa. Tukiwafikia wasusi, tutakuwa tumefikia maelfu ya familia kupitia wateja wao," amesema.

Kwa upande wake Meneja Mauzo wa Oryx Tanzania Shaban Fundi amesema kampuni hiyo imeamua kushirikiana na Kidoti Foundation kwa kutambua kuwa makundi ya kijamii yenye ushawishi yanaweza kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi nchini.

“Mbali  na kutoa suluhisho la nishati safi, kampuni yetu itaendelea kujenga uelewa wa wananchi kuhusu faida za matumizi ya gesi na teknolojia nyingine za kisasa zinazochangia kulinda afya na mazingira,”amesema na kusisitiza Oryx Gas na Kidoti Foundation kupitia makubaliano yanakwenda kuongeza watumiaji wa nishati safi nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCST Ntuli Mwakatobe amesema amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu ya kuwawezesha wanachama wa chama hicho kuwa sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya nishati safi nchini.

Amesema wasusi na wamiliki wa saluni wamekuwa wakitafuta njia za kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara zao huku wakihakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama zaidi.

"Leo tunapata nafasi ya kutumia nishati safi lakini pia kuwa sauti ya kuelimisha jamii. Hii ni fursa ambayo tutaenda kuitumia kuwafikia wateja wetu kila siku," amesema.

Matumizi ya nishati safi ya kupikia yanatajwa kuchangia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa unaochochea mabadiliko ya tabianchi, sambamba na kuboresha maisha ya wanawake ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakibeba mzigo mkubwa wa shughuli za kupikia.

Post a Comment

0 Comments