Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Louis Peter Bura akifungua mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa kikundi cha mafundi wanaojihusisha na uchomeleaji vyuma na useremala katika Kijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe, Wilaya ya Chato Mkoani Geita.
*********************
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Louis Peter Bura, amesema kasi kubwa ya ukuaji wauchumi katika Mkoa wa Geita imepelekea uhitaji wa huduma za usalama na afya mahalipa kazi kuongezeka ambapo ameutaka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuhakikisha upatikanaji wa huduma za ukaguzi na ushauri wa masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.
Ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa kikundi cha mafundi wanaojihusisha na uchomeleaji vyumana useremala katika Kijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe, Wilaya ya Chato MkoaniGeita.
Mafunzo hayo ambayo ni sehemu ya utekelezaji mpango mkakati wa Taasisi ya OSHA yametolewa Ijumaa (28/08/2026) kwa watu 15 ambao ni wanakikundi cha Smart Welders and Funirtures ambao kituo chao kimekuwa kikitumika kutoa mafunzo yaufundi kwa wananchi wa Kata ya Nyamirembe na maeneo ya karibu.
Mkuu wa Wilaya huyo amesema kwa kipindi cha miaka mitatu tangu mwaka 2024, Wilaya ya Chato imeshuhudia ongezeko kubwa la shughuli za kiuchumi zikiwemo shughuli za uchimbaji madini.
“Kipekee niwashukuru sana OSHA kwa kuendelea kutekeleza ipasavyo jukumu lenu la msingi la kusimamia usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini. Lakini naomba niwakumbushe kwamba maeneo mengi yanayokuwa kiuchumi yanahitaji sana huduma zenu ambapo Mkoa wa Geita hususan Wilaya ya Chato ni miongoni mwa maeneo hayo,” ameeleza Mheshimiwa Bura na kuongeza:
“Hivyo, niwaombe kuangalia maeneo haya kwa jicho la pekee kwani huko nyuma mlikuwa hamjulikani lakini kwasasa watu wanawatambua umuhimu wenu na wanahitaji huduma zenu za ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya, uchunguzi wa afya za wafanyakazi, mafunzo na ushauri wa kitaalam juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi.”
Aidha, DC Bura amewapongeza OSHA kwa kutoa mafunzo na msaada wa vifaa kinga kwa kikundi cha mafundi ambao shughuli zao zinagusa maisha ya maelfu ya wakazi waWilaya ya Chato.
Ameahidi kuendelea kushirikiana na OSHA katika kuhamasisha wakazi wa Chato kuzingatia kanuni bora za usalama na afya katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazotekelezwa katika Wilaya hiyo huku akiwataka wamiliki wa maeneo ya kazikuwapa ushirikiano wataalam wa OSHA.
Meneja wa OSHA Kanda ya Ziwa, Lodgard Bishanga, amesema mafunzo husika yalikuwa na lengo la kuwajengea uelewa wa vihatarishi vya kiusalama na afya katikashughuli zao za ufundi pamoja na mbinu za kudhibiti vihatarishi husika.
“Sambamba na kupatiwa mafunzo, washiriki wamekabidhiwa vifaa kinga vya mfano yakiwemo makoti ya usalama, glovu, kofia ngumu na barakoa ambavyo vimegharamiwa na serikali kama sehemu ya kuendelea kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika shughuli za uzalishaji,” ameeleza Meneja Bishanga.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wakiwemo Lulinda Makoye Manyema na Neema Kalebo wameishukuru Serikali kwa kuwajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya kazini pamoja na kuwapatia vifaa kinga.
“Tumejifunza mambo mengi sana kupitia mafunzo haya ikiwemo jinsi ya kukuza na kulinda usalama tunapokuwa katika karakana zetu ikiwemo kuwa na mpangilio mzuriwa mashine na vifaa. Aidha, tumejifunza jinsi ya kutoa huduma ya kwanza endapo itatokea ajali katika shughuli zetu za kila siku,” ameeleza Neema Kalebo, mshiriki wamafunzo.
Meneja wa OSHA Kanda ya Ziwa, Lodgard Bishanga, akiwasilisha mada katika mafunzo ya kuwajengea uelewa wa vihatarishi vya kiusalama na afya mafundi wauchomeleaji vyuma na useremala katika Kijiji cha Kalebezo, Kata ya NyamirembeWilaya ya Chato.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Louis Peter Bura, akikabidhi vifaa kinga vilivyogharamiwa na Serikali kwa mafundi wa uchomeleaji vyuma na useremala katikaKijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe Wilaya ya Chato. Mafundi hao walipatiwa mafunzo ya usalama na afya kazini na OSHA na kisha kukabidhiwa vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na kofia ngumu, glovu, barakoa na makoti ya usalama.
Mwanakikundi cha Smart Welders and Funirtures, kilichopo Kijiji cha Kalebezo, Kata yaNyamirembe, Wilaya Chato, akionesha mfano wa matumizi sahihi ya vifaa kinga katika shughuli za uchomeleaji vyuma baada ya kushiriki mafunzo ya usalama na afya kazini yaliyotolewa na Taasisi ya OSHA kwa wanakikundi tajwa.
Wanakikundi cha Smart Welders and Funirtures, kilichopo Kijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe, Wilaya Chato, wakiwa katika picha ya pamoja na Meneja wa Kanda ya Ziwa wa OSHA, Lodgard Bishanga (wa kwanza kushoto) na Afisa Maendeleo Nyamirembe, Sarah Seizure Hamza (wakwanza kulia) baada ya kushiriki mafunzo ya usalama na afya kazini yaliyotolewa na Taasisi ya OSHA kwa wanakikundi tajwa.









0 Comments