Ticker

6/recent/ticker-posts

Mkurugenzi Mtendaji wa ADEM Ashiriki Warsha ya Uthibitishaji wa Uongozi wa Shule Afrika

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Maendeleo ya Usimamizi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid J. Maulid, anashiriki warsha ya uthibitishaji iliyoandaliwa na Kituo cha Afrika cha Uongozi wa Shule (ACSL) jijini Nairobi, Kenya, kuanzia tarehe 10 hadi 13 Februari 2026.

Warsha hiyo imewakutanisha wadau muhimu wa uongozi wa shule kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, wakiwemo watunga sera, watoa huduma za maendeleo ya kitaaluma, watafiti, viongozi wa shule, pamoja na maafisa wa elimu. Jukwaa hilo linatoa fursa ya kupitia na kuboresha matokeo ya utafiti wa ramani ya uongozi wa shule, kwa lengo la kuhakikisha usahihi, muktadha stahiki, na matumizi yenye tija.

Lengo kuu la warsha ni kupitia, kuboresha, na kuthibitisha matokeo ya utafiti huo kupitia mashauriano shirikishi yanayohusisha wadau mbalimbali. Mchakato huu unalenga kuhakikisha ushahidi uliokusanywa ni sahihi, unaaminika, na unaendana na mazingira halisi ya mifumo ya elimu katika nchi za Afrika.

Aidha, warsha inalenga kujenga umiliki wa pamoja wa matokeo hayo na kuyatafsiri kuwa vipaumbele vinavyoweza kutekelezeka. Matokeo yaliyothibitishwa yanatarajiwa kusaidia maboresho ya sera katika ngazi ya kitaifa, pamoja na kuongoza mifumo na vipaumbele vya kimkakati katika ngazi za kikanda na bara zima.

Matokeo hayo pia yatachangia kuimarisha utendaji wa uongozi wa shule, kuunda mwelekeo wa programu za maendeleo ya kitaaluma, kuongoza tafiti na uzalishaji wa ushahidi, pamoja na kukuza ushirikiano na uratibu wa juhudi za kuboresha uongozi wa shule barani Afrika.

ACSL inaratibiwa na mashirika manne ya Kiafrika — Chama cha Maendeleo ya Elimu Afrika (ADEA), Education Sub-Saharan Africa (ESSA), Jukwaa la Wanawake Waelimishaji Afrika (FAWE), na VVOB – Education for Development — kwa ushirikiano na Taasisi ya Mastercard Foundation. ADEM inashiriki kama mdau kupitia ushirikiano wake na VVOB.

Post a Comment

0 Comments